MKUU WA WILAYA SONGEA, AMALIZA MGOGORO WA MUDA MREFU WA ARDHI HUKO MSHANGANO-SONGEA
Mkuu wa Wilaya ya Songea Profesa Norman Sigalla 'King'
Na Andrew Mhaiki, Mwanaperamiho blog
MKUU wa wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma,
Profesa Norman Sigalla” King’ amemaliza mgogoro wa muda mrefu wa kugombea ardhi eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi na kulirejesha mikononi mwa wananchi wa kata ya Mshangano katika Manispaa ya Songea mkoani hapa.
Wananchi hao waliingia kwenye mgogoro wa kugombea ardhi hiyo na mmiliki wa hoteli ya Top One Inn, Pascal Msigwa ambaye inadaiwa
walibadilisha matumizi na kumpimia eneo hilo na
kumilikishwa na Manispaa ya Songea
Wakizungumza na Mwanaperamiho juzi Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Samweli Mbano alisema kuwa Serikali kupitia Kamishna wa ardhi nchini waliingia mkataba na kampuni ya ardhi Plan kuja kupima maeneo ya kata hiyo ya Mshangano kwa kutenga maeneo ya makazi na huduma za kijamii.
Alisema kampuni hiyo ya ardhi Plan ilipima eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2.591, ploti namba 911 mwaka 2010 ambalo lilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi katika mtaa huo wa Mshangano ambapo wamekaa kusubiri ofa yao kutoka Manispaa hiyo ili waanze kazi ya ujenzi wa shule yao, alidai cha ajabu eneo hilo wananchi wamepokonywa na kumilikishwa mfanyabiashara ambaye amekuwa akiwaonyesha kiburi cha fedha.
Alisema wananchi wa kata hiyo walichukua uamuzi wa kulitenga eneo hilo kutoka shule ya msingi, Luhira iliyopo katika kata hiyo kukabiliwa na msongamano wa wanafunzi ambapo katika
chumba kimoja cha darasa wanasoma zaidi ya wanafunzi 100 walidai kitu ambacho kimekuwa kikishusha maendeleo
yao ya masomo ya darasani.
Alisema wakati wakiendelea kufuatilia ofa yao ili waanze ujenzi wa shule yao ya msingi,
walishangaa kuona kiwanja hicho uongozi wa ardhi wa Manispaa hiyo umemmilikisha mfanyabiashara huyo anayemiliki hoteli ya Top One Inn ya mjini hapa,
Pascal Msigwa ambaye tayari alianza ujenzi katika kiwanja hicho kwa kujenga nyumba na wananchi wa mtaa huo kwa pamoja waliandamana kwa hasira na kwenda kubomoa kwa lengo la kuusubiri uongozi wa idara ya ardhi ikiwemo Mkurugenzi, Zacharia Nachoa ili waweze kuwacharaza viboko kama watakwenda katika eneo hilo.
Alisema wananchi wa mtaa huo walikuja kupandwa na hasira kutokana na usumbufu waliokuwa wakiupata wa kufuatilia suala hilo kwa uongozi wa Manispaa hiyo bila ya mafanikio wakati mfanyabiashara
huyo akiendelea na ujenzi , huku watoto wao wakiwa wanateseka kwa kusoma kwa
kurundikana katika chumba kimoja cha darasa wakati eneo lao limeporwa na mfanyabiashara huyo.
Mwenyekiti, Mbano alisema kabla ya wananchi hawajuchukua sheria mkononi ya kuandamana na kwenda kuvunja kwa kubomoa ujenzi wa nyumba ya mfanyabiashara huyo ambayo ilikuwa ikijengwa katika kiwanja hicho ambacho kilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi katika mtaa huo wa Mshangano, uongozi wa Serikali ya mtaa huo ulimwita mfanyabiashara huyo, ambaapo alikaidi kwa madai kiwanja hicho ni mali yake na amekipata kihalali.
Alisema walipofuatilia zaidi waliweza kubaini kiwanja hicho kimepimwa zaidi ya mara moja akiwemo mmiliki wa Top One Inn VTC, Msigwa ambaye amekabidhiwa Ofa na kumilikishwa kinyume cha sheria na Manispaa hiyo kupitia faili lenye namba STC 27243/ MKN kiwanja namba 48 ambacho kimetolewa Januari, 18, 2013 chenye ukubwa wa m2 24,000
ambacho leseni yake inaonyesha kwa ajili ya makazi ambacho amelipia gharama fedha taaslim Sh. 650,000 hadi kuja kukipata na kuweza kukimiliki .
Mmoja wa wananchi wa mtaa huo wa Mshangano, Emilian Haule alipohojiwa na Mwanaperamihoblog alisema maamuzi yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya hiyo ya Songea, Profesa Sigalla” King” yamekuwa sahihi na wanampongeza ya kuwarejeshea kiwanja hicho mikononi mwa wananchi wa Mshangano na imekuwa mfano kwa viongozi wengine hasa viongozi wa Manispaa hiyo ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea badala ya kufuata misingi ya
kisheria wanapotoa maamuzi.
Naye Meneja wa Ardhi Plan mkoani Ruvuma, Francis Mwafyoma alipohojiwa na alisema kufuatia sheria ya ardhi 4/1999 ambayo inasimamiwa na Kamishina wa ardhi nchini alidai eneo hilo linalogombewa kati ya Top One Inn VTC na wananchi wa Serikali ya mtaa wa Mshangano alidai uamuzi uliotolewa na Mkuu wa wilaya,
Profesa Sigalla “King” umekuwa sahihi utasaidia kuondoa urasimu na ubabaishaji kwa viongozi wa Manispaa ya Songea
Hata hivyo Mmiliki wa Top One Inn VTC, Bw. Pascal Msigwa alipohojiwa kwa njia ya simu yake ya kiganjani yenye namba 0754353672 alikiri kuwepo kwa mgogoro kati yake na wananchi wa mtaa wa Mshangano wa kugombea kiwanja ambacho ni mali yake na anakimiliki kisheria kutoka mwaka 2013.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ya Songea, Bw. Zacharia Nachoa alipotafutwa ofisini kwake ili aweze kuelezea sakata hilo hakuweza kupatikana baada ya kuambiwa na
mmoja wa watumishi katika ofisi hiyo yupo nje ya ofisi kwa kazi ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya maabara kwenye shule za Sekondari, huku Ofisa ardhi Mteule wa Manispaa hiyo,
Andason Mwamengo ameahidi kupambana na wananchi hao wa Mshangano, licha ya Mkuu wa wilaya hiyo kumaliza tatizo hilo kwa kurejesha ardhi hiyo mikononi mwa wananchi.
Mkuu wa wilaya hiyo ya Songea, Profesa Norman Sigalla” King” alipohojiwa ofisini kwake jana juu ya sakata hilo la kugombea kiwanja kati ya wananchi wa Mshangano na mfanyabiashara huyo alisema baada ya kukaa na viongozi wa Manispaa na wananchi wa Mshangano meza moja na kufuatilia nyaraka za pande zote alidai Msigwa hakufuata taratibu za kisheria katika kukipata kiwanja hicho.
MWISHO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni