Ijumaa, 10 Julai 2015

WANACHAMA WA KLABU YA MAJIMAJI WAJITOLEA  ZOEZI LA UKARABATI WA UWANJA WA MAJIMAJI

Na  Andrew  Mhaiki, Mwanaperamiho blog

WANACHAMA  wa klabu  ya  Majimaji ya  Songea, tawi  la Amshawasha  lililopo  Msamala mjini hapa  wamejitokeza  kufanyakazi za kujitolea katika kusaidia  ukarabati  wa uwanja wa Majimaji  katika kazi za  kusambaza  kifusi  cha  mchanga  na kupanda  nyasi(ukoka) ikiwa ni sehemu ya  kuwaunga mkono  wadau  wa soka katika harakati  zao  za kuhakikisha  uwanja huo unaotumika kucheza  ligi ya Vodacom msimu ujao

     Akizungumza  mjini hapa jana Mwenyekiti wa tawi hilo la Amshawasha, Salehe Shaweji  alisema  kuwa wanachama  wa klabu ya Majimaji tawi la Amshawasha  wamekuwa wakitekeleza kauli mbiu  ya mkoa ya "Ruvuma kwanza" ikiwa na lengo la kuhakikisha Ruvuma  inarejea  kwenye  ramani  ya soka kama ilivyo  kwa miaka nyuma,

    Alisema  tawi hilo limeungana na wadau wengine wa soka katika kazi ya ukarabati  wa uwanja huo wa Majimaji baada ya kubaini wamiliki wa uwanja huo ambao ni chama cha Mapinduzi(CCM) kususia kufanyakazi hiyo kwa kisingizio cha ukosefu wa fedha wakati  ligi ya Vodacom inakaribia kuanza Majimaji ikiwa miongoni mwa vilabu ambavyo vitakavyoshiriki ligi  hiyo hapa  nchini.

    Alisema  baada  ya kubaini  hilo wanachama wa tawi hilo kwa umoja wao waliamua kuhamasishana  na kwenda kufanya kazi hiyo ya kusambaza  kifusi cha mchanga pamoja na kupanda ukoka ikiwa moja wa mchango wao kwa klabu hiyo ya Majimaji huku akidai pamoja na zawadi kwa Wanaruvuma ambao wamekuwa na kiu kubwa ya kuhakikisha timu yao ya Majimaji  inatumia  uwanja huo kwenye mechi zake za nyumba kucheza ligi hiyo,

    Mwenyekiti huyo pia alisema pamoja na kuiona Majimaji ikicheza  kwenye uwanja huo bado kwa wafanyabiashara watakuwa na fursa nzuri za kiuchumi kwa kujiongezea  kipato cha kifedha wakiwemo wafanyabiashara  wa nyumba za wageni, mamalishe na wenye vyombo vya usafiri kutokana na kuwepo kwa wageni watakao kuja kuishuhudia Majimaji  ikicheza  nyumbani kitu  ambacho kimekuwa kikililiwa kwa mikoa ambayo haina timu inayoshiriki ligi kuu ya Tanzania Bara.


    Naye mlezi wa tawi  hilo la Amshawasha, Joseph Nswila alipohojiwa na mwandishi wa habari  hizi wakati wakiendelea na hilo zoezi la kusambaza kifusi na kupanda ukoka alisema tawi hilo lenye wanachama 60 limekuwa likifanyakazi  ya kujitolea pamoja na kuchangia  fedha  kwa ajili  ya Maendeleo ya klabu yao ya Majimaji, huku likifanya kazi ya kuhamasisha  wakazi wa mkoa wa Ruvuma  ndani na nje ya mkoa wahakikishe  Ruvuma inakuwa kimaendeleo kupitia soka kwa kutumia kauli ya mkoa ya " Ruvuma kwanza"

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni