HUU HAPA WASIFU WA Dkt. JOHN MAGUFURI, MGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA TIKETI YA CCM
AJIRA ya kwanza ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Joseph Magufuli (55) ilikuwa ni ualimu na atasherehekea siku yake ya kuzaliwa siku nne tu baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kwa mujibu wa wasifu wake uliogawiwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliomchagua kuwa mgombea juzi katika Ukumbi wa Mikutano wa CCM uliopo Dodoma, Magufuli alianza kazi akiwa mwalimu wa masomo ya kemia na hisabati katika Shule ya Sekondari Sengerema mkoani Mwanza.
Kwa maana hiyo, mgombea urais huyu ni mwanasayansi na kama atachaguliwa kuwa Rais wa Tano wa Tanzania kwa kuwashinda wagombea wa upinzania, basi atakuwa Rais wa kwanza mwanasayansi kuitawala Tanzania.
Marais waliomtangulia; Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete ni wasomi katika fani ya ama sanaa au uchumi, hakuna mwanasayansi.
Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 katika Wilaya ya Chato ambayo ni mojawapo ya wilaya tano za mkoa mpya wa Geita uliopo kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Wilaya ya Chato ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera na ni mwaka 2012 tu ndipo ilipohamishiwa Mkoa wa Geita.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Chato ina jumla ya wakazi 365, 127; huku wengi wao wakiwa na asili ya kabila la Wasukuma.
Magufuli alipata elimu ya msingi katika Shule ya Chato na masomo ya sekondari ya awali katika Seminari ya Katoke, Biharamulo. Alimalizia kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lake, mkoani Mwanza. Kidato cha sita alimalizia katika sekondari ya Mkwawa mkoani Iringa.
Wasifu wa Magufuli unaonyesha kwamba alipata cheti cha Stashahada ya Ualimu katika Chuo cha Elimu Mkwawa mnamo mwaka 1982 – alikojikita zaidi katika masomo ya hisabati na kemia.
Kati ya mwaka 1985 hadi 1988, Magufuli alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya masomo yake ya shahada ya kwanza ya ualimu wa kemia na hisabati.
Waziri huyo wa Ujenzi alijipatia shahada yake ya uzamili kwenye kemia kupitia Vyuo Vikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Salford cha Uingereza kati ya mwaka 1991 na 1994.
Wakati akiwa waziri katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2009, Magufuli alijiunga na UDSM alikosomea Shahada ya Uzamivu katika kemia (PhD-Chemistry).
Magufuli aliingia katika Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza mwaka 1995 wakati alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, na hajawahi kukaa nje ya baraza hilo tangu wakati huo.
Amewahi kuwa waziri katika wizara tofauti kama vile Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mwanasiasa huyu ni mwanataaluma mbobezi, akiwa tayari ni mwanachama wa vyama vya kitaaluma kama Chama cha Wakemia wa Tanzania na kile cha Wataalamu wa Hisabati Tanzania.
John Joseph Pombe Magufuli ana mahaba na namba. Si kwamba amesoma hisabati kama somo lakini amekuwa akipenda masuala ya namba na moja ya alama yake kubwa ya kiutendaji ni uwezo wake mkubwa wa kukariri takwimu mbalimbali kuhusu masuala anayoyafanyia kazi.
Kama msomi, Dk. Magufuli ameandika machapisho mbalimbali yakiwamo; “A New Rate Equation for Solid State Decomposition and its Application to the Decomposition of Calcium Carbon Trioxide, The Control and Management of Heat as Challenge and Opportunity to Engineers, Funding for the EAC Road Network Project na The Potential of Anacardic Acid Self-Assembled Monolayer From Cashew Nut Shell Liquid As Corrosion Protection Coating (2009).
Mke wa Magufuli, Janet, ni Mwalimu wa Shule ya Msingii Mbuyuni, shule aliyokuwa akifundisha Salma, mke wa Rais Jakaya Kikwete.
Sifa nyingine ya ziada ya John Pombe Magufuli ni kwamba hanywi pombe wala havuti sigara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni