PAULO
MALDINI: BEKI MSTAARABU ZAIDI AMBAYE HAKUWAHI KUPATA KADI NYEKUNDU UWANJANI
Na Oswald Ngonyani
Mchezo wa
mpira wa miguu maarufu kama soka bado umeendelea kuwa mchezo pendwa kwa watu
wengi zaidi kote duniani na hata kuizidi michezo mingineyo kinaganaga. Ni
mchezo unaopendwa na watu wa kariba zote.
Kutokana na
mchezo huo kuhusudiwa na watu wengi zaidi tayari kumekuwepo na wachezaji fulani
fulani ambao kwayo wamejipatia umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wao ndani ya
dimba. Wachezaji hhawa wapo wengi sana lakini kwa leo nitamzungumzia mchezaji
wa nafasi ya ulinzi ambaye enzi zake aliwahi kuwakonga mashabiki wengi wa wa
mchezo wa soka.
Namzungumzia
muitaliano Paulo Maldini ambaye majina yake kamili ni Paolo Cesare Maldin aliyewahi kuwa
mchezaji wa kariba ya juu zaidi katika mawanda ya soka la kimataifa akicheza
katika nafasi ya ulinzi wa pembeni (left back) au nafasi ya ulinzi wa kati
(central defender). Alizaliwa tarehe 26 Juni mwaka 1968 huko Milan nchini
Italia. Katika enzi zake alihudumu katika misimu 25 akisakata kabumbu katika
Ligi Kuu ya nchini Italia maarufu kama Serie A.
Ana kimo cha mita 1.86 akiwa ni Baba wa watoto wawili
Christian Maldini na Daniel Maldini. Alistaafu kuichezea timu yake ya Taifa
mwaka 2002 ambapo katika nyakati zake za kuuchezea mpira aliweza kukiongoza
kikosi cha Italia kwa miaka 8 akiwa kama nahodha wa timu hiyo iliyowahi kutwaa
ubingwa wa kombe la dunia mara nne. Anaaminika kuwa mlinzi bora zaidi wa miaka
yote katika soka la dunia.
Aliwahi kupata tuzo ya UEFA ya mlinzi bora wakati akiwa na
miaka 39 lakini pia tuzo ya mlinzi bora wa Ligi ya Serie A mwaka 2004. Mara
kadhaa jina lake liliwahi kujumuishwa katika kikosi cha wachezaji bora wa dunia
na hata kuzidi kuchagiza ukulu wake katika mawanda ya usakataji wa kabumbu.
Akiwa ndiye
beki bora zaidi katika enzi zake, ni vigumu kuamini kuwa mlinzi huyu kisiki hakuwahi
kutwaa tuzo ya Ballon d’Or hasa mwaka 1994 ambapo akiwa na AC Milan aliiwezesha
klabu hiyo kutwaa Serie A, Supercoppa Italiana, Ligi ya Mabingwa Ulaya na UEFA
Super Cup, lakini hakupewa tuzo ya Ballon d’Or. Mwaka huo huo aliiongoza Italia
kushika nafasi ya pili katika Fainali za Kombe la Dunia na kutangazwa kuwa
mchezaji bora wa dunia na gazeti la World Soccer, lakini tuzo ya Ballon d’Or
ilichukuliwa na raia wa Bulgaria, Hristo Stoichkov aliyekuwa akiichezea klabu
ya Barcelona.
Mwaka 2002
alishiriki kwa mara ya nne fainali za kombe la dunia na fainali za pili akiwa
kama kapteni wa timu yake ya Taifa ni katika mwaka huo Maldini alikuwemo katika
kikosi cha wachezaji 11 waliochaguliwa kuunda kikosi cha dunia kilichojulikana
kwa jina la ‘FIFA World Cup dream team”
Ndani na nje ya
uwanja wachezaji wenzake walimchukulia Maldini kama kiongozi wao. Si katika
timu yake ya Taifa pekee lakini pia katika klabu yake aliyowahi kuichezea kwa
mahaba makubwa AC Milan ambapo mpaka sasa mashabiki wa klabu hiyo wangali
wakimkumbuka.
Ni mchezaji wa
kiwango cha kimataifa aliyecheza soka lake katika klabu moja pekee. Alishinda
mataji 26 wakati wa uchezaji wake wa muda wa misimu 25. Mlinzi mwepesi, mgumu
kupitika aliyekuwa na uwezo wa hali ya juu wa kufanya maamuzi sahihi awapo
uwanjani.
Anashikilia
rekodi ya kucheza michezo mingi ya michuano ya
Vilabu Ulaya akiwa amecheza michezo 174, ikiwa ni pamoja na kufunga goli
la mapema zaidi katika fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya mwaka 2005 goli la
sekunde ya 50 katika mchezo dhidi ya Liverpool, mchezo ambao pamoja na timu
yake ya AC Milan kutangulia kwa goli 3-0 mwisho wa siku uliamuliwa kwa mikwaju
ya penalti baada ya akina Steven Gerald kusawazisha magoli hayo na baadaye
kuutwaa ubingwa huo.
Maldini
amewahi kuvaa medali tano za European Cup katika miaka ya 1989, 1990, 1994,
2003 na 2007 kitu ambacho si kidogo katika mawanda ya usakataji wa kabumbu kwa
mchezaji yeyote yule. Alikuwa ni mmoja kati ya walinzi bora zaidi katika
historia ya Ligi ya mabingwa Ulaya
lakini pia alikuwa akivutia sana kutokana na ukweli kwamba alipokuwa na
mpira ilikuwa ni vigumu kumdhania kuwa ni yeye kutokana na ukweli kwamba staili yake ya
kiuchezaji haikutofautiana na mchezaji wa sehemu ya kiungo.
Ikumbukwe kuwa kama si George Weah wa
Liberia kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia mwaka 1995 basi huenda tuzo hiyo
ingekwenda kwa Paulo Maldini ambaye alishika nafasi ya pili huku Jurge
Klinsmann wa Ujerumani akishika nafasi ya tatu.
Ni miongoni mwa wachezaji waliowahi
kuifanyia makubwa timu ya Taifa ya Italia kama ilivyo kwa akina Dino Zoff, Paolo Maldini na Silvio Piola.
Ukulu wake katika usakataji wa ‘Gozi la Ng’ombe’ ungali ukikumbukwa tena na
tena na wanafamilia wa mchezo wa soka ulimwenguni kote.
Alikuwa na kipaji cha pekee ndani ya dimba ambapo mbali na
sifa zote nilizozielezea hapo juu, Maldini alikuwa na uwezo wa kutumia miguu
yote miwili (wa kulia na kushoto) kama ilivyo kwa akina Andreas Brehme, Pavel
Nedvěd, Toni Kroos, Adriano Correia na Julian Draxler ambao Mwenyezi Mungu
aliwapa uwezo wa kutumia miguu yote katika kuuchezea mpira.
Kuna mengi sana ya kuandika kuhusu mlinzi huyu maarufu ambaye
kwa bahati mbaya hakuwahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia. Lakini
kikubwa zaidi ambacho kinapaswa kukumbukwa ni historia yake nzuri kuhusu mchezo
wa soka, historia iliyotukuka, historia ambayo inazidi kuchagiza ukulu wake
tena na tena, historia ya kucheza kandanda pasipo kupata kadi nyekundu mpaka
anastaafu.
Naomba
kuwasilisha…..
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni