Jumapili, 21 Juni 2015

MAONI: HAWA NDIO WATAPITISHWA NA CCM URAIS 2015
Image result for kikwete
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Tanzania anayemalizia muda wake.

Na Shedrack Sinyenga, Peramiho
Kama Kamati Kuu ya CCM itaamua kusimama kwenye Kanuni za uchaguzi na utaratibu usio rasmi, kuna nafasi moja tu ambayo imebaki kwa wagombea waliobaki 31+ ili kuungana na wagombea wanne ambao wanabebwa na kanuni na pia utaratibu usio rasmi katika maamuzi ya Kamati Kuu.

Ikumbukwe Kamati Kuu ya CCM huteuwa majina 5 na kuyapeleka kwenye Halmashauri Kuu ambayo huteuwa majina 3 na kuyapeleka kwenye Mkutano Mkuu ili uteuwe jina 1 la mgombea Urais.

Kwa utaratibu usio rasmi ndani ya CCM, hakuna mwana CCM anaruhusiwa kupambana na Rais anayeomba kugombea tena kwa muhura wa pili. Uchaguzi huu, hakuna Rais anayeomba kugombea.
Kwa utaratibu usio rasmi ndani ya CCM, Makamu wa Rais anayeomba kugombea Urais lazima apitishwe na Kamati Kuu ili akapigiwe kura kwenye NEC. Tulishuhudia mwaka 1995 kwa Mzee Cleopa David Msuya. Kwa maana nyingine, lazima jina la Makamu wa Rais wa Tanzania, Mohamed Gharib Bilal atakuwa ni miongoni mwa majina 5.

Kwa utaratibu usio rasmi, Waziri Mkuu pia lazima awepo kwenye majina matano. Tulishuhudia mwaka 1995 kwa Mzee Cleopa David Msuya na mwaka 2005 kwa Fredrick Tluway Sumaye, kwa maana nyingine, Mizengo Kayanda Pinda atakuwa miongoni mwa majina matano.

Kauli mbiu ya CCM inasema, wanawake wakiwezeshwa wanaweza, ndiyo maana hata kwenye Katiba Inayopendekezwa kuna 50-50 za nafasi kati ya wanaume na wanawake (gender equality). Kwa kulitambua hilo, Kamati Kuu itaweka jina la mwanamke kwenye majina matano, kwa maana nyingine, Dr Asharose Migiro atakuwa miongoni mwa majina matano. Usiniulize kwa nini, sababu unazifahamu!

Kwa kutambua umuhimu wa Muungano na kujenga mshikamano ndani ya CCM, Kamati Kuu itateuwa majina mawili ya wana CCM kutoka Zanzibar. Hii ni kusema Judge Augustine Ramadhani ataungana na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal ili kukamilisha idadi ya Wazanzibari wawili . Usiniulize kwa nini, sababu unazifahamu!

Kwa kifupi, haya ndiyo majina yatakayopelekwa na Kamati Kuu kwenye Halmashauri Kuu hapo tarehe 10 Julai 2015. 
1) Dk. Mohamed Gharib Bilal 
2) Mizengo Kayanda Pinda. 
3) Dr Asharose Migiro. 
4) Judge Augustine Ramadhani. 
5)...? 

Kwenye orodha hii, kuna Watanzania Bara 2 na Wazanzibari 2 
Wana CCM zaidi ya 31 kwa sasa wanapambana kwenye nafasi 1 ili waungane na niliowataja hapo juu ili wakapigiwe kura kwenye Halmashauri Kuu. Hii nafasi 1 itakuwa ni nafasi ya mwana CCM kutoka Tanzania Bara ili kutengeneza uwiano unaoeleweka.

(Shedrack Sinyenga ni Mwandishi Mwandamizi wa Blog hii anapatikana kwa simu namba 0756 08 55 35)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni