Jumanne, 23 Juni 2015

ETI  TUWAPE NCHI WAKOMESHE "RUSHWA", WAFUFUE "VIWANDA", "KILIMO".........?


Na Shedrack Sinienga

Tatizo walilokuwa nalo Wamarekani wengi miaka ya 1800 hadi kufikia 1860’s ilikuwa ni UTUMWA, na hii ilikuwa ni kero kubwa sana kwa Wamarekani weusi na hata Wamarekani weupe wachache baadhi ya majimbo. Ilikuwa ni tatizo kubwa sana kutokana na kitendo chenyewe cha utumwa kuwa si jambo la kibinadamu. 

Hili tatizo halikupata kabisa kiongozi mwenye dhamila ya dhati kabisa kuliondoa kwa zaidi ya miaka 70 kwa Wamarekani Weusi. Jambo hili lilipigiwa sana kelele wakati Franklin Pierce alipokuwa Rais wa 14 wa nchi hiyo 1853–1857. Bahati nzuri sana Rais aliyefuatia yaani rais wa 15 tena alikuwa wa Democratic kama alivyokuwa mtangulizi wake naye hakulifanyia kazi jambo hili, huyu si mwingine bali James Buchanan, Jr. 1857–1861. 

Likazidi kugawa Taifa. Wakati anamaliza muda wake mawazo ya wengi yalipingana na misimamo yake, na chama chake kikawa na mpasuko mkubwa. Kutokana na uwezo wake mdogo wa kuweza kuwaleta pamoja Wamarekani waliokuwa wakipinga Utumwa kukomeshwa na wale walikuwa wanataka utumwa usikomeshwe ilisababisha mvurugano ndani ya nchi. Kufuatia hayo yote sasa wananchi wakapoteza matumaini na chama cha Democratic kwamba hakitaweza kutatuwa matatizo yao hasa kukomesha utumwa. 

Tunapofika leo hapa sisi kama Watanzania tunajambo la kujifunza, tena kubwa sana. Ukiangalia nyuma kwa makini utaona hawa ni sawa na Wamarekani walioshindwa kukomesha Utumwa kwa zaidi ya miaka mingi sana. Lakini kumbe nyuma yake walikuwepo watu wenye maono na uwezo wa kukomesha kabisa hali hiyo ya utumwa. 

Ilipokuwa imefika 1860, hali majadala wa utumwa nchini Marekani ilikuwa ya moto sana, ni vipi vyama vya siasa vingekabiliana na hali hiyo na kudumisha umoja wa kitaifa? Bahati nzuri sana huu ulikuwa ni wakati wa Abraham Lincoln kutoka chama cha Ripublican na sera zake za kukomesha utumwa. Hata aliungwa mkono na wa Democrat wengi sana na kwasababu alikuja na mawazo mapya wakamuamini wakamuchagua.

Leo hii kati ya Marais maarufu Marekani huyu ni mmoja wapo. Amepata umaarufu huo sababu moja tu aliweza kukomesha utumwa Marekani wakati wa kipindi cha uongozi wake. Anaheshimika sana na Taifa hilo kubwa duniani na hata duniani kote. 

Nasisi wakati huu tunahitaji kuwapima wagombea wetu kwa kina sana hasa hawa ambao wamekuwa viongozi wetu kwa muda sasa. Tuangalie Je, hawa kweli wataweza? Wakati wa ahadi umepitwa na wakati. Nitajenga Shule, Nitaleta viwanda, ooohhoo! Ajira kwa vijana!!!! Wengi tunapenda kusikia ni vipi utayafanya haya? Uchumi unatokana na kazi za watu zenye tija.

Kitu kikubwa ambacho naweza kusema hapa ni kwamba tupo kwenye wakati wa mpito lakini wakati tunapita hapo tunahitaji kujihoji sana. Je, tupite hivihivi tulivyozoea kupita?
Watanzania tumekuwa na matatizo mengi sana karibu miaka 30, Umasikini, Afya, Ajira, Maji, Umeme, Miundombinu, michezo, Kilimo, Elimu n.k. Je, hawa wote wanaotuambia watayatoa haya kweli tujiulize bila ushabiki wowote ule wa kisiasa WATAWEZA kuyakabiri? Na kwa namna gani watayafikia hayo? La, haya yote yamekuwa chini yao na kukomaa chini yao hivyo hivyo yataendelea kustawi chini yao. Wawapishe wengine warudishe heshima ya nchi.

Ukweli mabadiriko tunayataka lakini hayawezi kupatikana ndani ya hawa ambao wamekuwa na mawazo yaleyale na sura zilezile daima. 
Kwa mawazo yangu mimi sitaki Serikali ifanye kila kitu kwa wananchi wake, bali Serikali ifanye mambo yale ambayo Wananchi hatuwezi kufanya mfano, “Kuleta maji safi na salama kwa wananchi”, “Kuboresha huduma za Afya”, “Kulinda wananchi”, “Kujenga miundombinu mizuri ya elimu” na mambo mengine mengi ambayo yataleta tija katika ustawi wa jamii. Lakini ukikuta Serikali inakuwa chanzo cha matatizo ya wananchi inanipa mashaka sana kama tunaweza kuwa salama.

Wakati tulio sasa Serikali za namna hii zimepitwa na muda, tunahitaji mabadiriko makubwa. Sijui tumekuwa tukifanya namna gani tangia vyama vingi ama “CHANGE MANAGEMENT” au “CHANGE OF MANAGENT.” Ingawa kuna tofauti lakini naona tumekuwa tukifanya kitu kilele tangu uhuru. Yatupasa tubadirike sana mwaka huu, na uhakika kabisa nje ya sura zilezile tutapata kiongozi mwenye weledi mkubwa sana wa kusongesha taifa hili mbele.

Niseme ukweli tu hapa. Laana iliyowakuta Wamarekani wakati wa utumwa na hata ukiangalia jambo lenyewe lilivyokuwa si nzuri mbele ya macho ya Mungu kuwatumikisha binadamu kama wanyama na sisi imetufika. Utumwa ni sawa tu na kutotenda haki kwa watu wako hata kama huwatumikishi kinguvu. Kama wewe unaweza kuiba ama kufisidi mali ya Umma unautofauti gani na Mmarekani mweupe aliyewatumikisha wafrika weusi kwa ujira mdogo? 

Kama wananchi wanalipa kodi ili waweze kuboreshewa huduma zao za kijamii alafu wewe unatumia kodi hizo kwa manufaa yako binafsi, unautofauti gani na hao waliouza utu wa mtu na kumtumikisha? Kama unaweza kujenga barabara mbovu watu wakapata ajari wakafa unautofauti gani na wale weupe wamarekani waliowakata watumwa mikono na miguu? Kama unaweza kuhujumu miundombinu ya maji ili wananchi wasipate maji safi na salama huna utafauti na mkoloni.
 
Kama unaweza kutengeneza dawa za binadamu feki, huna utofauti na Mmarekani aliyekuwa anawafanyisha kazi ngumu watumwa bila kuwapa chakula. Sasa nasisi laana imetufika.

Naiona laana hii kwetu. Pamoja na wote waliotia nia kuwa ni Mawaziri na kujinasibu kuwa wanataka kuletea maisha mazuri, kutuleta kwenye uchumi wa kati. Napata taabu sana hata wanashindwa kutetea yanayotokea Bungeni, huwezi kuwa makini hata kidogo unapunguza Pay as you earn 1% alafu unaongeza tozo ya mafuta ya taa ya Tsh 50. Wakati wananchi wengi ndo wanatumia mafuta. Kweli tuko makini? Mbona mnatudanganya mchana kweupe. 

Sitabiri na mimi si mtabiri lakini naona anguko kubwa kama Democrat ya Marekanki mwaka 1860 iliyopelekea hadi nchi kuingia kwenye machafuko sababu ya watu wachache waliokuwa ndani ya utawala kushindwa kwenye uchaguzi lakini hawakukubali kuachia madaraka na kujaribu kuigawa nchi. 

Kupata viongozi wa nchi jamani ni mchakato, hamuwezi kutwambia kwamba nchi hii sasa kila mtu anaweza kuwa kiongozi. Twambieni tu nyie mmemuandaa nani? Kupiga miruzi mingi hii ni kutuchanganya, na sitaki kuamini kuwa hamna mtu, mnae mleteni sasa msiogope tunataka kumjua mapema sana na tuweze kutafakari vizuri nae.

Mungu atubariki soooote!
Maoni/Ushauri tuma kwenda 0756085535 au kwa barua pepe shedisoft@yahoo.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni