UMEFANYA
MENGI IKER CASSILAS, DUNIA ITAKUKUMBUKA
DAIMA DUMU
Na
Oswald Ngonyani
Kinaweza kikawa kipindi kigumu zaidi kwa mashabiki wengi
wa klabu kongwe na tajiri ya nchini Hispania, Real Madrid, klabu ambayo
ilianzishwa mwaka 1902 na kujikusanyia idadi kubwa ya mashabiki pande zote za
dunia.
Pengine ukongwe na umaridadi wa klabu hiyo ni miongoni
mwa vitu vingi vilivyo nyuma ya siri ya kuwa na upana wa mashabiki lakini
umaarufu na uwezo wa wachezaji wake ndani ya dimba ni sababu nyingine yenye
mashiko zaidi.
Binafsi ninaweza kuandika mambo kadha wa kadha kuhusu
ukulu wa klabu ya Real Madrid, lakini
sitakuwa muungwana iwapo sitamtaja mlinda mlango mahiri wa muda mrefu wa klabu
hiyo na timu ya Taifa ya Hispania, Comrade Iker Cassilas.
Shujaa huyu wa muda mrefu pale jijini Madrid hayupo
katika wakati mzuri kwa sasa. Ni wazi kuwa shaka yake juu ya kinachoendelea
klabuni hapo kwa sasa hivi inachagizwa na uwepo wa Mwalimu mpya klabuni hapo,
Rafael Benitez.
Mwalimu huyu aliyekabidhiwa mikoba yote ya Carlo Ancelotti
ameonekana kuwa sababu ya hiki kinachuzungumzwa sasa kuwa nyanda huyu ni lazima
aondoke klabuni hapo ili magolikipa wengine chipukizi waweze kutua klabuni hapo
na hata kuenenda na mifumo inayotakiwa chini yake.
Ni ukweli ulio wazi kuwa huwezi kuyazungumzia mafanikio
ya sasa ya klabu ya Real Madrid pasipo kumzungumzia mlinda mlango huyu ambaye
kwa muda mrefu sasa ameitumia vema kandarasi yake ya mchezo wa soka akiwa na
klabu hiyo.
Ni ngumu sana kwa mchezaji yoyote duniani kufikia ndoto
nyingi na kubwa kama ilivyo kwa Casillas. Lakini kwa bahati mbaya sana nyanda
huyu anakwenda kuihama klabu hiyo aliyoitumikia kwa mahaba makubwa huku akiwa
hajatimiza ndoto moja ambayo alikuwa amejiwekea ndani ya moyo wake.
Nakumbuka wakati fulani kwenye mahojiano fulani ambayo yalifanyika
mwaka uliopita (Oktoba 2014) ilithibitika kwamba Cassilas alikuwa na ndoto kubwa
katika maisha yake, ndoto ya kucheza soka ndani ya Madrid na kumaliza hapo
hapo.
Alizungumza maneno haya “Real Madrid ni nyumbani kwetu,
Sikuwahi kuwa na majirani sana au hata vikundi vya shuleni. Nilikuwa na miaka 8
nilivyoanza kucheza mashindano na wakati nina miaka 9 walinisaini.
Nilikuja
hapa kwa hatua na napaona hapa ni nyumbani kwetu. Siku zote nimekuwa sehemu ya
Madrid na nimekuwa kama mchezaji na binadamu wa kawaida kwa malezi ya hapa
hapa. Mimi nimekuwa hapa na kuwa na kumbukumbu zote hapa hapa”
Iker alisema kwamba sio rahisi na vigumu kumuona yeye akiwa
ndani ya jezi ya timu nyingine, “Ni vigumu kufikiria mimi katika timu nyingine.
Nitastaafu mpira nikiwa hapahapa. Japokuwa ningependa kujaribu ligi nyingine
ili niweze kujua changamoto za kwingineko lakini kwangu mimi Madrid ni chaguo
la kwanza zaidi kwani huko hakutakuwa kama hapa.”
Maneno tajwa ya hapo kati yanaonyesha namna ambavyo
mwanandinga huyu mwenye miaka 34 alivyo katika ‘dilemma’ hivi sasa kwani
mabadiliko ya Kocha yanaonekana kuikatiza ndoto yake ya siku nyingi tangu
anajiunga na klabu hiyo miaka 25 iliyopita.
Ni wazi kuwa nyuma ya kila kinachoendelea hivi sasa
kuhusu golikipa huyu yupo mtu mmoja ambaye Uongozi mzima wa Klabu ya Real
Madrid umemuamini, mtu huyu si mwingine bali ni Kocha mzawa aliyekulia klabuni
hapo Rafael Benitez Maudes maarufu kwa jina la Rafa Benitez.
Hapana shaka kuna kitu kimoja kipo ndani ya ubongo wa
Mwalimu huyu, kitu ambacho ni vema mashabiki wengi wakakijua ili kutokosa
majibu pale watakapoona mchezaji wao kipenzi Iker Cassilas anaenenda zake.
Kwa miaka nenda rudi kumekuwepo na dhana ya wachezaji
fulani kuwa ndio mhimili wa klabu hiyo, mhimili ambao kwayo umekuwa ukipewa
sana nafasi katika vichwa vya bodi nzima ya Ukurugenzi wa klabu hiyo lakini pia
mashabiki husika.
Wapo wachezaji wengi ambao wamewahi kupitia katika ukulu
huu pale Madrid. Miongoni mwa wote waliwahi kupikwa katika chungu hiki cha
kutukuzwa yupo pia Iker Cassilas ambaye sasa hivi ustahimilivu wake pale Madrid
upo shakani.
Ni ukweli uli wazi kuwa Cassilas ambaye alikabidhishwa
kofia hiyo ya ukulu kutoka kwa mkongwe wa siku nyingi wa klabu hiyo Raul
Gonzalez, yu mbioni kuondoka zake, sababu ni moja tu, hajawa chaguo sahihi la
Benitez.
Ndoto yake haitaweza kutimia tena. Ilianza kuyumbishwa
tangu enzi za Jose Mourinho, kwa bahati nzuri akaja Carlo Ancelotti ambaye
alimfanya kuwa golikipa wa chaguo la kwanza katika mechi za mashindano makubwa
kama UEFA na Copa De Ley nafasi ambayo aliifanyia mambo makubwa na hata kuzidi
kujiongezea sifa ya kuaminika klabuni hapo.
Baada ya miaka 25 ya kukaa kwenye klabu yake hiyo
hatimaye siku zake kwenye timu hiyo zimetimilika. Kipa huyu ambaye alikuwa
kwenye tetesi nyingi za kuhama klabuni hapo nafasi yake kwa sasa ni ndogo sana
klabuni hapo.
Ripoti za uhakika ni kwamba Real Madrid na F.C Porto
wamefikia makubaliano ya msingi na na ni wazi kuwa msimu ujao wa Ligi atacheza
soka yake nchini Ureno.
Kwa vyovyote vile ni wazi kuwa mpambanaji huyu wa miaka
mingi pale Madrid itampasa kuondoka zake japo mazuri yake klabuni hapo
yataendelea kukumbukwa tena na tena. Linaweza likawa ni pigo kubwa kwa Rais wa
timu hiyo Florentino Perez lakini hakuna namna kwani kocha waliyempa kandarasi
mpya klabuni hapo yupo nyuma ya kila kinachoendelea kwa sasa.
Ngoja tusubiri
tuone………………
(0767 57 32 87)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni