COPA
AMERIKA 2015: ILIKUWA NI FAINALI YA ALEXIS SANCHEZ NA LIONEL MESSI.
Na Oswald Ngonyani.
Dunia nzima ilikuwa kimya
kushuhudia mchezo wa fainali wa Mashindano ya Copa America ambapo timu mwenyeji
ya Chile ilikuwa inapambana na timu ya Taifa ya Argentina, mchezo ambao
ulitabiriwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na uimara wa kila timu.
Haukuwa mchezo wa
lelemama, ulikuwa ni mchezo ambao kila Taifa lilikuwa linataka kuweka heshima
fulani, heshima ambayo mwisho wa siku ingeweza kuleta kumbukumbu ya pekee
katika historia ya mchezo wa soka katika bara husika. Ilikuwa ni vita ya akina
Lionel Messi, Angel Di Maria na wengineo dhidi ya akina Alexis Sanchez na
wenzake waliokuwa wanaunda kikosi cha Chile.
Kunako
mchezo huo uliopigwa Usiku wa kuamkia Jumapili iliyopota Chile walifanikiwa kuweka
historia mpya kabisa wakiwa nyumbani,
baada ya kupata ushindi mnono wa goli 4-1, ushindi wa mikwaju ya penati na
kutwaa ubingwa huo mkubwa katika ngazi ya mabara.
Hili ni
kombe la kwanza kutwaa nyumbani katika historia ya soka yao, ambapo wakati
Alexis Sanchez wa Arsenal aliyeng’ara tangu mwanzo akicheka hadi mwisho, Lionel
Messi wa Argentina alikumbana na kigingi na hata kukumbwa na fadhaiko kuu ndani
ya moyo wake.
Haikuwa
mechi ya masihara, ilikuwa ni mechi iliyoonekana kuwa ngumu kwa kila timu na
ndio maana dakika 90 za awali zilionekana kuwa ngumu kwa timu zote mbili,
lakini hata zilipoongezwa dakika nyingine 30 bado milango ilionekana kuwa
migumu na hivyo changamoto ya mikwaju ya penalti kuchukua nafasi yake.
(Alexis Sanchez akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la ushindi na kuipa ubingwa wa kwanza wa Kombe la Copa America)
Alikuwa
ni Alex Sanchez aliyepeleka furaha nchini Chile baada ya kupiga mkwaju wa ushindi na
kushangilia kwa muda mrefu huku wenzake wakijumuika naye kumsapoti.
Usiku
huo haukuwa mzuri kwa Higuain hii ni kutokana na ukweli kuwa katika dakika ya
90 alishindwa kufunga bao la wazi ambalo lingemaliza mchezo katika muda wa
kawaida. Wakiwa suluhu walilazimika kucheza dakika 30 za nyongeza lakini hakuna
aliyebahatika kufumania nyavu za mwenzake, lakini hata katika hatua ya matuta
bado Higuin aliendeleza mkosi baada ya penalti yake kutoingia nyavuni.
Sanchez
naye nusura afunge katika dakika za mwanzo za muda wa nyongeza lakini ilibidi
wafike hatua za matuta ili mshindi aweze kupatikana. Ni Messi peke yake ndiye
aliyeweza kutikisa nyavu za wapinzani, wanzake wote wala hawakuweza kufunga
penati zao na hata kuzidi kumpa machungu mwanandinga huyo aliye na kiu ya kuipa
mafanikio nchi yake.
Ikumbukwe
kuwa Timu ya Taifa ya Argentina, au Le Albiceleste kama wanavyojulikana kwa
utani, hawajatwaa taji kubwa kwa miaka 22 sasa, kwani mara ya mwisho walitwaa kombe
hili walilobeba Chile nchini Ecuador mwaka 1993.
(Fainali ya Copa America mwaka huu 2015 ilifanyika hapa)
Kwa
upande wa mabingwa wapya, hii ni mara yao ya kwanza kutwaa kombe hili katika
kipindi cha miaka 99 na nusura imalizike karne pasipo kulitwaa. Hata hivyo,
kutokana na uimara wa kikosi chao, wengi walisema wakikosa safari hii huenda
ikabaki historia.
Chile
ni moja ya timu zilizocheza mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa 1916
nchini Argentina lakini walichoweza kufanya vyema zaidi ilikuwa ni kupata
ushindi wa pili, ambao wameutwaa mara nne; 1955, 1956, 1979 na 1987.
Kimahesabu
ya mchezo wa soka ni kwamba akina Alexis Sanchez na Artulo Vidal wametwaa
ubingwa huu baada ya kucheza mechi 173 katika mashindano yote, yaani tangu
mashindano ya kwanza ya Copa America mwaka 1916.
Kunako
mchezo huo Chile hawakucheza kwa kushambulia kama ilivyokuwa imezoeleka kabla,
hii ilitokana na umaridadi wa kikosi cha Argentina, hivyo walichofanya ni
kuwavuta Argentina, huku wakicheza kwa nidhamu ya hali ya juu lakini mara moja
moja walifanya mashambulizi ya kushtukiza yalikuwa yanaongozwa na nyota wao Sanchez na Charles Aranguiz.
Washabiki
wao walikuwa wakishangilia mwanzo mwisho kwenye fainali hiyo kwa lengo la
kuchagiza ushindi waliokuwa wameukosa kwa miaka mingi, walipeperusha bendera
zao nyekundu ili kuwapa morali wachezaji wao waliokuwa wanacheza nyumbani.
Kila timu ilifunga penati ya kwanza, Matias
Fernandez akitia yake kwenye kona ya juu kwa Chile kabla ya Messi kuingiza yake
kima cha chini kwenye kona.
Hata
hivyo, baada ya kiungo wa Juventus, Arturo Vidal kupiga mkwaju mkali na kujaa
wavuni kwa Chile, Higuain alipiga juu ya mwamba; Aranguiz akafanya mabao kuwa
3-1 ndipo Banega akazuiwa na Bravo huku Sanchez akicheka na nyavu na kuanza ‘shamra
shamra’ ya aina yake ndani na nje ya uwanja.
(Kikombe cha ubingwa wa Copa America 2015 kilichokuwa kinagombaniwa katika fainali hiyo)
Ni
kama kusema Argentina wamenyang’anywa tonge la pili mdomoni, baada ya mwaka
jana 2014 kuukosa ubingwa wa dunia
katika fainali ambazo kikosi chao kilionekana kuwa bora zaidi kama cha msimu
huu, wajerumani walitamatisha ndoto zao baada ya Mario Goitze aliyeingia
kipindi cha pili kucheka na nyavu kunako dakika za lala salama.
Bila
shaka matokeo haya yameendelea kumuumiza sana Lionel Messi, mchezaji wa kiwango
cha hali ya juu aliyechukua kila kikombe ndani ya Klabu yake ya Barcelona, kwa
bahati mbaya hajafanya hivyo kwa timu yake ya Taifa. Bila shaka nyakati hizi
huenda zikaathiri sana maisha yake ya ndani na nje ya uwanja.
NGOJA TUSUBIRI TUONE…….
(Maoni/Ushauri tuma kwenda
0767 57 32 87 au ngonyanioswald@gmail.com)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni