MARADONA & PELE: WALIWAHI KUIKONGA DUNIA NA
KUANDIKA ALAMA ISIYOFUTIKA KATIKA VICHWA VYA WAPENDA SOKA WENGI ULIMWENGUNI
Inaendelea
kutoka Makala ya juzi……
DIEGO
ARMANDO MARADONA
Diego Armando Maradona alizaliwa tarehe 30Mwezi Oktoba 1960, ni mchezaji maarufu wa mpira wa miguu aliyewahi kuwika sana katika kikosi cha timu yake ya Taifa ya Argentina.
Ana urefu wa Mita 1.65 ambaye katika enzi zake za
kusakata Gozi la ng’ombe alikuwa akicheza katika nafasi ya ushambuliaji wa
kati. Katika nyakati fofauti yaani kati ya mwaka 1976 mpaka 1997 aliwahi
kuvichezea vilabu vy Argentina Juniors, Boca Juniors, Barcelona, Napoli,
Sevilla, na Newell’s Old Boys, huku akiwa tegemezi katika timu yake ya Taifa
katika miaka ya 1977-1994.
Mchezo wa soka kama unavyojidhihirisha kwa kuwa
na ubora wa hali ya juu na hata kujikusanyia mashabiki wengi kuliko michezo
mingineyo umekuwa ni zaidi ya mchezo wa kawaida. Hauna tofauti na sanaa. Kwa baadhi ya watu mchezo wa soka
ni imani kama ilivyo imani nyingine za dini. Kuna watu akili na mawazo yao siku
zote vimeathirika na soka.
Ndivyo ilivyo kwa wakazi wa Taifa la Argentina,
Taifa ambalo kwayo mchezo wa soka hauna tofauti
na dini au imani. Kwa
wenyewe mwanaume huyu ‘Diego Maradona’
ni kama Mungu wao. Mambo yote aliyowahi kuyafanya enzi zake za usakataji wa
kabumbu na hata sasa baada ya kustaafu kwao ni mambo yaliyowekwa katika viriba
vya ubongo wao na kamwe hawatakuja kuyasahau.
Ni kama kusema kuna wafuasi wengi sana wa dhehebu la Maradona ndani na
nje ya Argentina hususan Amerika. Diego Armando Maradona hana tofauti na nabii
aliyetokea kupendwa sana lakini pia kuchukiwa sana na jamii ya wapenda soka
ulimwenguni kote. Hapa ndipo anapotofautiana
na nguli mwingine wa kandanda, Pele wa Brazil.
Kwa jinsi ilivyo ni wazi kuwa hakuna shabiki wa
soka atakayeweza kunipinga iwapo nitaandika sentensi hii ‘Ni wanasoka wachache
sana katika ulimwengu huu wa kandanda waliotokea kuibua hisia za wapenzi wa
mchezo huo kwa namna ya pekee kama ilivyo kwa Maradona’. Huo ndio ukweli.
Japo sikuzaliwa lakini takwimu za soka
zinanifanya niweke bayana kuwa uwezo wa Maradona na umahiri wake katika kuuchezea
mpira ulionekana wazi zaidi katika mwaka wa 1986 katika michuano ya Kombe la
Dunia na hususan katika pambano la Argentina dhidi ya Uingereza.
Mpaka leo hii waingereza wamegoma kabisa
kumsamehe Maradona. Pengine wana sababu
nyingi zinazowafanya wamjengee ‘bifu’ la milele
lakini sababu kubwa ni hii; Maradona alifunga goli la mkono, lakini
baadaye kidogo Maradona alifunga goli la kiufundi na la utalaamu wa hali ya juu
zaidi pale alipoambaa kwa kasi na mpira akitokea nusu ya uwanja.
Jemedari huyu aliwapiga chenga za maudhi karibu
wachezaji wote wa Uingereza waliomkabili. Kisha aliukwamisha mpira kimiani.
Kilikuwa ni kitendo cha aibu kubwa sana kwa wachezaji wa Uingereza kwao ni kama
aliwafedhehesha na hata kuonekana si kitu mbele ya halaiki ya mashabiki wao
waliojitokeza kuangalia mchezo huo nchini Mexico.
Maradona alidhihirisha umahiri wake katika sanaa
ya kandanda, sanaa inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wafuasi. Itakumbukwa,
kuwa Argentina ilishinda Kombe la Dunia mwaka ule., ni wazi kuwa goli la mkono
lilichagiza kuivusha Argentina katika hatua iliyofuata, mpaka leo waingereza
bado wana kinyongo na nabii huyu wa soka.
Miaka minne baadae, juhudi binafsi za Maradona
ziliiwezesha nchi yake kushika nafasi ya juu zaidi katika michuano ya Kombe la
Dunia. Huu ni ukulu mwingine wa Maradona, ukulu ambao unamfanya azidi kuheshimika
zaidi katika mawanda ya kandanda.
Katika fainali zile mechi kati ya Brazil na
Argentina ndiyo iliyokuwa na kivutio cha pekee. Brazil waliwazidi Argentina
katika idara zote, hivyo basi, Argentina na Maradona wao wala haikupumua.
Lakini ajabu iliyoje, kama radi, kama gharika, Mwanamume huyu alizinduka na
kuishangaza dunia ya wapenda soka wengi duniani waliokuwa wakifuatilia mchezo
ule.
Akiwa amebanwa katika kila upande huku akikabwa
na walinzi wa Brazil, Maradona alifanikiwa kutoa pasi muhimu katika maisha yake
ya yote ya kisoka.Ilikuwa pasi murua kwa mchezaji mwenzake, Claudio Caniggia
ambaye alifunga goli pekee katika mchezo huo.
Argentina waliingia fainali na kushindwa mbele ya
wababe wengine wa soka ‘Ujerumani’. Kama hiyo haitoshi, Fainali za Kombe la
Dunia za mwaka 1994 zilimshuhudia Maradona akiwa katika hatua za kuporomoka
kisoka. Nabii huyu wa soka sasa likuwa ameanza kupoteza mvuto.
Alijitahidi kidogo katika mechi za awali, kisha
likalipuka bomu lililomharibia kabisa sifa yake ya kuwa juu kisoka na hata
kumpa mwanya mpinzani wake, Edson Pele kuonekana bora zaidi kuliko yeye.
Maradona alibainika kutumia vidonge vya kuongeza
nguvu aina ya efedrin. Argentina nayo ikapoteza mvuto mbele ya washika dau
wengi wa kandanda lakini pia haikufanya cha maana katika hatua za awali za
fainali hizo.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Nabii Maradona, nabii
wa soka anayezungumzwa zaidi mpaka sasa. Soka kama dini ina wafuasi wengi sana
ambao si rahisi kuwahesabu. Siku zote bila mpira uwanjani hakuna soka. Kama ulivyo
mpira wenyewe, una umbo la mviringo, wenye sura nyingi zisizoelezeka na wenye
kudunda, basi hata pambano lenyewe la soka laweza kuwa na sura nyingi. Ndiyo
maana watu husema Mpira unadunda, hii maana yake ni kwamba katika soka lolote
laweza kutokea.
Soka, kandanda, kabumbu, kipute au ndinga. Yote
hayo na mengineyo ni majina yenye kuzungumzia aina moja ya mchezo ambao si
mchezo mwingine bali ni mpira wa miguu.
Kwangu mchezo huu ni kama mchezo wa maajabu, Tazama, katika mchezo huu
mchezaji anaruhusiwa kutumia sehemu nyingine zote za mwili, kichwa, kifua,
tumbo, makalio,mgongo, kisigino na hata
kidevu, lakini kamwe haruhusiwi kutumia mkono.
Tofauti na michezo mingine kama Wavu, Kikapu,
Mpira wa meza na mingineyo mingi ambapo mikono hupewa kipaumbele zaidi katika
kila mchezo. Ajabu iliyoje, Ni dhambi kubwa sana katika soka kwa mchezaji wa
soka kuucheza mchezo huo kwa kutumia mkono na kibaya zaidi akifanya hivyo kwa
kudhamiria, kwa makusudi. Dhambi hiyo haisameheki katika soka, adhabu yake ni
kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Mkono ni Ibilisi wa soka.
Ndio maana mpaka leo hii, Waingereza hawatakoma
kumlaani Diego Maradona wa Argentina kwa kufunga goli lile la mkono
nililolielezea katika aya za mwanzoni.
Kwa Waingereza, Maradona alifunga goli kwa
kumtumia Ibilisi wa soka, wana haki ya kumlaumu kwani safari yao nchini Mexico
katika mwaka ule (1986) iliishia hapo kwa goli la mkono wa Maradona.
Maradona mwenyewe alitoa kauli ambayo ilizidi
kuwanyong’onyesha Waingereza alipodai kuwa lilikuwa goli la mkono wa Mungu!
(0767 57
32 87)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni