NIMEMKUMBUKA MARC VIVIAN FOE, NABII WA SOKA ALIYEIFIA TIMU YAKE AKIWA
ANAPAMBANA UWANJANI
Na
Oswald Ngonyani

(Pumzika kwa amani Marc Vivian Foe, Familia ya wapenda soka duniani kote itakuenzi daima dumu)
Tarehe Mosi Mwezi Mei
mwaka huu 2015, familia ya soka duniani kote ilifanya kumbukizi ya pekee ya
kukumbuka miaka 12 ya kifo cha
mpambanaji Marc Vivian Foe, Kijana aliyefariki ghafla uwanjani akiwa
analitumikia Taifa lake la Cameroon nchini Ufaransa.
Jasiri huyu aliyekuwa na umri wa miaka 28 kwa wakati huo
alianguka katika zulia la uwanja wa Stade Gerland mjini Lyon nchini Ufaransa na
kuzua hali ya sintofahamu miongoni mwa mashabiki wengi wa soka.
Baada ya majaribio ya kumfufua kufeli, aliondolewa
uwanjani kwa machela huku matabibu kadha wa kadha wakitumia dakika 45 kujaribu kuyanusuru
maisha yake kabla ya kuieleza dunia kuwa mpambanaji huyo alikuwa amefariki
dunia.
Kijana huyu aliyetokea katika familia masikini kwenye
kijiji kimoja cha Nkolo nje ya mji wa Younde, alijikuta akilala usingizi wa milele
huku wachezaji wenzake wakiongozwa na nahodha wa kikosi hicho nyakati hizo
Rigobert Song wakiandamwa na simanzi.
Ilikuwa ni hali iliyozua ukimya wa muda mrefu katika
nafsi za wapenzi wengi wa kandanda ulimwenguni kote. Wakameruni walikuwa
wamempoteza mchezaji wao, kipenzi chao Marc Vivien Foe.
Alizaliwa tarehe Mosi Mwezi Mei mwaka 1975 huko Younde nchini
Cameroon. Alianza soka akiwa na klabu ya daraja la pili ya Union Garoua kabla
hajahamia kwenye klabu ya Canon Yaoundé, moja ya timu kubwa nchini Cameroon.
Alianza kung`ara tangu
alipoitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon mwaka 1993 na kuwafanya mawakala
na makocha wa vilabu kadhaa barani Ulaya kuanza kuitafuta saini yake mwaka 1994
kwenye fainali za kombe la dunia nchini Marekani.
Kifo chake kiliishitusha
dunia ya wapenda kandanda wengi, kwani ilikuwa ni ghafla mno. Ilikuwa kwenye
michuano ya kombe la mabara mwaka 2003 tena katika hatua ya nusu fainali wakati
Cameroon ikicheza na Colombia ambapo kunako dakika ya 72, Foe alidondoka
katikati ya dimba na juhudi za kuokoa maisha yake ziligonga mwamba.
Nakumbuka kunako mwendelezo
wa mashindano hayo, mshambuliaji Thiery Henry wa Ufaransa alishangilia goli
lake kwenye mechi ya pili ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuonyesha vidole
juu kama ishara ya kumkumbuka Foe, ambapo kabla ya mchezo huo wachezaji wengi
walitokwa na machozi kwa kumpoteza mwenzao.
Hata katika mchezo wa
fainali, Baada ya Thiery Henry kufunga,
manahodha Marcel Desailly na Rigobert Song waliinua kombe pamoja huku baadhi ya
mashabiki wakiinua mabango yaliyosomeka hivi: “Simba huwa hafi, huwa analala
tu.”
Foe alifariki dunia kwa
kile kilichodaiwa kuwa ni mshituko wa moyo. Nchini Cameroon Foe alipewa mazishi
ya kitaifa na heshima zote, ambapo Serikali ilisimamia gharama zote za mazishi.
Ni miaka kumi na miwili sasa tangu Foe aanze safari ambayo kila aendaye
huwa harudi. Imeendelea kuwa simanzi isiyofutika katika nyoyo za wapenda soka wengi
asilani. Marc Vivien Foe shujaa
aliyewahi kupewa
tuzo ya kamanda wa taifa la Cameroon, alifia vitani, alifariki dunia akiwa
anaipigania nchi yake huku mashuhuda wa kifo chake hicho wakibaki midomo wazi.
Alilifia Taifa lake akiwa anapambana uwanjani. Alikata
kauli akiwa anaitumikia Timu yake ya Taifa kwa dhati ya moyo wake lakini wala
hakufikia hatma aliyokuwa anaitegemea, Mwenyezi Mungu aliamua kumchukua.
Ingawa ni kipindi kirefu kidogo tangu nchi ya Cameroon na
Afrika ikumbwe na gadhabiko hili la nafsi, Taifa hilo bado halijakuwa katika
kiwango kile ambacho kilikuwepo katika enzi na nyakati za Foe.
Fainali za mwaka jana (2014) zilizofanyika nchini Brazili
ni ushahidi tosha wa namna ambavyo Taifa hili limekuwa la kawaida mno katika
mawanda ya usakataji wa Gozi la ng’ombe tofauti na miaka ile ya 2000’s.
Leo hii dunia ya wapenda soka inapomkumbuka mpambanaji
huyu ni lazima itataka kujua mustakabali wa mchezo wa soka nchini humo kwa
sasa, kitu ambacho ni wazi kuwa kitawafanya wasimanzike nyoyo zao kutokana na
ubora wa Taifa hilo katika soka kuzidi kuwa chini.
“A Lion
Never Die, He Just Lays There Sleeping” Ama kwa hakika Simba huwa hafi, analala tu
chini kupumzika. Pumzika kwa amani Marc Vivien Foe, wewe mbele yetu sisi
nyuma yako! Tutazidi kukuenzi sasa na hata siku zijazo….! Amina.
Maoni/Ushauri tuma kwenda (0767 57 32 87) au
ngonyanioswald@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni