NIDHAMU MBOVU KWA WACHEZAJI, MASHABIKI NA HATA VIONGOZI INAHARIBU UTAMU WA LIGI MBALIMBALI PERAMIHO
Na Oswald Ngonyani
Mchezo wa mpira wa miguu maarufu kwa jina la Soka, ni mchezo ambao bado umeendelea kuwa na idadi kubwa ya mashabiki kuliko michezo mingine yote inayochezwa katika hii dunia tunayoishi.
Ni mchezo ambao umeonekana kuziteka nyoyo za watu wa kariba zote na hata kuzidi kujipatia nyongeza ya mashabiki kila jua linapochomoza. Unapendwa na Wazee, Vijana, na hata watoto. Watu wa rika na jinsia zote ni wafuasi wakubwa wa mchezo huu, ni mchezo unaohusudiwa pia na watu wa kada na matabaka tofauti.
Kama ilivyo kwa wakazi wa maeneo mengine ya ndani na nje ya Tanzania, wakazi wa mji wa Peramiho nao pia ni wanazi wakubwa wa mchezo wa soka. Ushahidi wa nadharia hii upo wazi kwani katika kila Ligi inayofanyika katika viunga vya ndani ya mji huu, idadi ya wanaojitokeza kushuhudia michezo hiyo ni mamia kwa mamia.
Pengine mwitikio huu wa watu wa kariba na rika zote katika mahaba yao kwa mchezo wa soka ndio haswaa uliopelekea wadau mbalimbali wa mji huu wa kihistoria kuandaa mabonanza na matamasha ya mchezo wa soka lakini pia kuna ambao kwa dhati ya mioyo yao wamekuwa wakiendesha Ligi zao kila mwaka kwa lengo la kutoa fursa kwa vijana wa Peramiho lakini pia kutoa burudani kwa wakazi wa ndani na nje ya Peramiho.
Leo hi ni kitu tulichokwisha kukizoea kuhusu uwepo wa Ligi mbalimbali ambazo tayari zimekwishaweka alama isiyofutika katika vichwa vya wapenda soka wengi wa hapa Peramiho.
Uwepo wa Ligi kongwe ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Peramiho Dk. Ansgar Stuffe OSB inayojulikana kwa jina la KOMBE LA PASAKA au ANSGAR CUP lakini pia uwepo wa Ligi iliyoanza katika miaka ya karibuni (NJUNDE CUP) ni miongoni mwa vitu ambavyo vinazidi kuleta burudani kwa wanaperamiho wengi hivi sasa.
Sasa hivi kila wikiendi na siku za katikati ya juma watu wanapata burudani halisi na hata kushuhudia viwango vya hali ya juu ambavyo wala havitofautiani sana na viwango vya wachezaji wanaocheza Ligi kuu ya Vodacom (VPL).
Leo hii uwapo katika Uwanja wa Tamasha (Namihoro) mahali muafaka ambapo mashindano ya NJUNDE CUP yanafanyika utapata wasaa wa kupata burudani murua za uwezo wa wachezaji ndani ya dimba.
Pengine mapana ya usajili ndio haswaa sababu msingi ya mashindano haya kuonekana kuwa matamu zaidi. Kwani wapo wachezaji wa timu kubwa hapa nchini ambao wanatumiwa na Ligi hii na hivyo kuzidi kutia nakshi ya ubora kwa mashindano haya.
Kwa bahati nzuri, mimi binafsi nimekuwa mfuasi mkubwa wa Ligi mbalimbali za hapa Peramiho na kwa asilimia kubwa nimekuwa nikiwa katika jopo la Viongozi wanaoongoza na kuratibu mashindano haya.
Nimekuwa nikijifunza mengi kutoka kwa Viongozi wenzangu, wachezaji lakini pia kwa mashabiki wa timu husika na hata kuwa na mengi ya kuyaandika ama kuyazungumza pale ninapotakiwa kufanya hivyo.
Huwa sisiti kuuzungumza ukweli pale inapobidi, na katika hilo tayari nimekwishawahi kukosana na Viongozi fulani wakubwa wa Ligi fulani baada ya kuuzungumza ukweli fulani Katika Kipindi cha Michezo cha TBC Songea ambao kwayo hawakuwa tayari kuelezwa ukweli hata kama walikuwa wamekengeuka.
Ninasema walikuwa wamekengeuka kwa sababu sikuona hoja za msingi kutoka kwao ambazo ziliwatuma kunishutumu kwa ukweli niliokuwa nimeuzungumza, pengine walipotoshwa na dhana ya ya miaka nenda rudi ya kufanya mambo kwa mazoea pasipo kukosolewa.
Siku zote sisi wanahabari huwa tunausimamia sana mhimili mmoja ambao ndio dira ya Uanahabari wetu. Mhimili huo si mwingine bali ni dhana ya ukweli. Hii ina maana kuwa jambo lolote lenye kweli ndani yake ni ruksa kuliweka bayana haijalishi limefanywa na nani, ndivyo ninavyopenda kufanya na katika hilo sitaweza kutikisa masikio ama kupepesa macho. Nitaeleza ukweli kwa kila itakaponibidi kwa lengo lengwa la wafuasi wa mchezo wa soka wa ndani na nje ya Peramiho.
Lengo la maandishi yangu haya kwa siku ya leo si kuwazungumzia Viongozi hao ambao ninawahifadhi kwa majina, lengo la makala haya elimishi ni kuzibeza baadhi ya tabia za watu fulani fulani ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa kiini cha matatizo mengi yanayotokea uwanjani wakati wa mechi fulani fulani.
Jana Jumapili kulikuwa na mechi za mwendelezo wa mashindano ya NJUNDE CUP kwa mechi za Kundi B iliyozikutanisha timu za CHICAGO FC kutoka Likuyu iliyokuwa inapambana na MAGIMA FC kutoka Kata ya Litisha.
Ulikuwa ni mchezo uliokuwa na ‘tension’ kubwa kutokana na kila timu kuitafuta nafasi ya kuingia hatua ya nusu fainali katika mashindano hayo yanayoonekana kuteka nafsi za wapenzi wengi wa kandanda hapa Peramiho.
Kwa bahati nzuri sana nilikuwa Kamisaa wa mchezo huo na kwa kweli niliyashuhudia mambo mengi ambayo binafsi nina watu ambao ninaamini kuwa walikuwa sababu ya kile ambacho kilikuja kutokea baadaye.
Tangu kuanza kwa Mashindano haya, sisi kama Kamati ya kuendesha Ligi (mimi na wanakamati wengine) tuliazimia kuwatumia marefarii watoto ambao wana leseni ya uamuzi wa mchezo wa soka baada ya kuhudhuria mafunzo ya awali ya uamuzi mwaka jana (2014).
Haikuwa mara ya kwanza kwa watoto hawa kuchezesha mechi za mashindano kwani tuliwatumia pia katika mashindano ya KOMBE LA PASAKA (ANSGAR CUP) kwa ngazi ya Kata ambapo walionekana kuchezesha kwa weledi mkubwa na hata kuhusudiwa na wanaperamiho wengi wanaopenda kandanda.
Binafsi, uwezo ambao umeoneshwa na mabwana wadogo hawa kwa mtazamo wangu unazidi ule wa marefariii ambao tumewazoea na ambao miongoni mwao kuna mmoja amekuwa akipandikiza chuki ya wazi kwa mashabiki wa kandanda kwa kuzipotosha sheria 17 za mchezo wa soka ili angalau wadogo hawa waonekane wanakosea ili yeye aweze kupata nafasi ya kuchezesha kitu ambacho sidhani kama tutakuja kukifanya.
Pengine kauli hizo za upotoshaji zilichagiza kumjaza ujinga mlinda mlango wa CHICAGO FC ya Likuyu Bw. Greyson Maseko ambaye katika dakika ya 69 ya kipindi cha pili alifanya kitendo cha utovu wa nidhamu ambacho sidhani kama atakuja kukisahau katika maisha yake yote ya usakataji wa kabumbu.
Kwanini hatakuja kusahau? Mchezaji huyu ambaye mimi ninamwita ‘mjinga’ alimpiga refarii wa kati kwa kile alichokuwa anaamini kuwa goli ambalo alikuwa amefungwa halikuwa sahihi.
Pengine uhalali wa goli lile ndiyo sababu iliyowafanya mashabiki wengi wamkimbilie na kwenda kumfunda adabu, alipigwa na wengi kwa ujinga aliokuwa ameufanya na hata kujikuta akiwa akipelekwa Kituo cha Polisi kwa kosa lisilo la kiuanamichezo la kumpiga mwamuzi.
Binafsi ninamuona mtu fulani nyuma ya maamuzi ya golikipa huyo, mtu ambaye anajulikana na wengi kama kiini cha mchezo wa jana kuingiwa na dosari lakini pia mashabiki fulani fulani ambao siku zote huwa wanakuja uwanjani kwa lengo la kuleta fujo.
Hapana shaka ushawishi wa mtu huyo lakini pia ushawishi wa mashabiki hao wajinga umemponza mlinda mlango huyo ambaye sidhani kama jamii ya wapenda soka wengi wa Peramiho itakuja kumsamehe.
Kwa mtu mzima kama yeye kumvamia mtoto mdogo wa miaka 15 na kumpiga ni kitendo ambacho hakiwezi kuungwa mkono na binadamu yeyote aliye na akili timamu.
Kwa mtu mzima kama yeye kumvamia mtoto mdogo wa miaka 15 na kumpiga ni kitendo ambacho hakiwezi kuungwa mkono na binadamu yeyote aliye na akili timamu.
Tena unamvamia refarii kwa goli la halali kama lile, unataka mashuhuda wa mchezo huo wakufanye nini? Si lengo langu kuwasifu walioamua kuingia uwanjani na kumuadabisha mlinda mlango huyo lakini kwa ujinga aliokuwa ameufanya hakuna ambaye angeweza kuvumilia.
Mwisho wa siku ninarudi pale pale kuwa wakati mwingine nidhamu mbovu za Viongozi wetu, lakini pia Wachezaji na mashabiki wa mchezo husika ndiyo sababu ya Ligi zetu nyingi kuharibika.
Ili kuenenda na mantiki halisia ya FIFA (Shirikisho lenye dhamana ya mpira wa miguu duniani) ya ‘Fair Play’ ni wakati muafaka kwa kila mtu kuwa muumini mkubwa wa nidhamu awapo uwanjani, Kinyume na hapo huenda tukapunguza idadi ya wadau wengine wa kandanda ambao pengine walikuwa na nia ya kuanzisha Ligi kama hizi hapo baadaye.
Michezo ni Afya, Michezo ni Upendo. Hakuna haja ya kuwekeana uadui kwa kitu ambacho ukweli wake upo wazi. Bahati nzuri sana mchezo huu unachezwa hadharani na kushuhudiwa na kila anayekuwepo uwanjani hapo.
Ni jukumu ka kila shabiki wa mchezo wa soka hapa Peramiho kujitafakari upya katika nafsi yake kuhusu ushiriki wake uwanjani, Je unaleta tija kwa wengine au unawabugudhi wengine? Hapana shaka kwa kufanya hivyo tutakuwa tunasafiri katika chungu kimoja cha mafanikio ya soka Peramiho.
Siku zote ninaamini katika ukweli, huwa sitikisi masikio wala kupepesa macho inaponibidi kuuzungumza ama kuandika. Ninaamini somo langu hili limeeleweka vema.
Maoni/Ushauri tuma kwenda namba 0767 57 32 87/0673573287, au kwa barua pepe kwenda ngonyanioswald@gmail.com, mwanaperamiho@gmail.com! Pia waweza kunisoma katika Gazeti la Michezo la Dimba kwa siku za Jumatano na Jumapili, lakini unaweza kutembelea www.mwanaperamiho.blogspot.com

(MAELEZO YA PICHA: Nikiwa na Mwenyekiti wa NJUNDE CUP Bw. Ausy Maulid ofisini kwangu Peramiho Publications)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni