NIMEKUWEKEA UHONDO WA WIKIENDI KUTOKA KWA MWANAPERAMIHO
JINA LA HADITHI: MISS PERAMIHO (Mlimbwende wa Peramiho)
MTUNZI/MWANDISHI: Oswald Ngonyani
MAWASILIANO: 0767573287 au ngonyanioswald@gmail.com
MWAKA WA KUANDIKWA: 2013/2014
SURA YA KWANZA: (Vivian Matata)
“Siamini, Siamini tena siamini kabisaaaa!” (Vivian alitamka kwa jazba)
“Kwanini huamini Vivy?, kipi kinakufanya usiamini mpenzi” (Vanessa aliuliza kwa msisitizo)
“Vane! Vane shosti wangu wa ukweli hivi ni kweli Vivian mimi nimekuwa Miss Peramiho? Is it true?”
“It is true Vivy, ulikuwa na vigezo vyote vya kuwa mlimbwende wa Peramiho, waliokuwa wakikupondea walikuwa na chuki binafsi tu na ndio maana mara tu baada ya kutangazwa kwako kuwa mshindi kila mtu aliyekuwa ukumbini kushuhudia fainali zile alipiga makofi na kushangilia kwa sauti kubwa, hii maana yake ni kwamba ulikubalika na kila mtu, na hata jina lako lilipotangazwa hakuna hata mtu mmoja aliyeonekana kushangaa, Wewe ni Miss halali wa Peramiho Vivy, believe me or not”
“Sijui, Sijui Vanessa, mpaka sasa sijui ninini kilifanyika kwani kwa jinsi mashindano haya yalivyokuwa yakiendeshwa na waratibu wake na kwa jinsi nilivyokuwa katika wakati mgumu hata sikuwaza kama nitakuja kushinda taji hili”
“Hayo yalikuwa ni mapito tu Vivy wangu, nadhani Mwenyezi Mungu aliamua kuingilia kati ili haki iweze kutendeka ndio maana hata walimbwende wenzako uliokuwa unapambana nao walionekana wakikupigia makofi kukushangilia hii maana yake ni kwamba uliwazidi katika kila idara”
“Unasemaje Vanessa?”
“Ninasema hivi kila penye nia pana njia, isitoshe Mwenyezi Mungu akipanga jambo kamwe haliwezi kupanguliwa na binadamu yeyote, ninamaanisha kuwa ushindi wako ulikwishapangwa na Mola aliye juu na kwa hakika ni lazima ungeshinda tu taji hili hata kama wangechakachua mwisho wa siku ukweli ungejulikana tu, Vivy rafiki yangu You are Miss Peramiho, Wewe ndiwe mlimbwende wetu wa Peramiho ni lazima ulikubali suala hili majaji wa mashindano haya wala hawakukosea, umesikia?”
“Nimekusikia na nimekuelewa vizuri rafiki”
“Kama umenielewa mimi ninashukuru”
Vivian Matata na Vanesa Solomon wanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Maposeni mkoani Ruvuma walijikuta wakiwa katika kikao kisicho rasmi nje ya Ukumbi wa Posta ukumbi maarufu kuliko kumbi zote za mjini Peramiho, kikao hicho kilifanyika mara tu baada ya fainali za kumtafuta mrembo wa Peramiho kufikia ukomo fainali ambazo ziliwafanya watu wakeshe mpaka majogoo huku msichana mrembo Vivian akiibuka kidedea.
Utaratibu wa kiutendaji hasa katika kuyaendesha mashindano hayo ndio haswa uliopelekea wasichana hawa wazuri kujikuta wakiwa katika kikao hicho hasa kwa lengo la kuwekana sawa ikiwa ni pamoja na kujengana kisaikolojia kwani Vivian alikuwa haamini kama ni kweli alikuwa Mlimbwende mpya wa Peramiho ambaye alizawadiwa zawadi nono zilizokuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni kumi za kitanzania.
******
Taarifa kuhusu ushindi wa Vivian Matata zilionekana kumpendeza kila mkazi wa Peramiho na vitongoji jirani, kwani uzuri wa sura aliokuwa nao ulimfanya awe maarufu na kujikuta akijijengea jina kubwa ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma, uzuri wake haukuwa wa kawaida na haikuwa rahisi kuuelezea.
“Nasikia mwanafunzi wetu ameshinda taji la Miss Peramiho kwa mwaka huu”
“Ndiyo, tena nasikia amevunja rekodi yaani tangu mashindano haya yaanzishwe hajawahi kupatikana mrembo aliyeumbika kama Vivian Matata"
Unasema kweli Mwalimu?”
“Huo ndio ukweli kwani hujasikiliza redio asubuhi?”
“Mwenzangu, unadhani nina mazoea ya kusikiliza redio basi?’
“Shauri lako, ungesikiliza ungesikia sifa za mwanafunzi wako, nasikia ametia fora kweli kweli”
Yalikuwa ni mazungumzo ya walimu wake na Vivian Matata baada ya kusikia taarifa za ushindi wake kupitia kituo cha redio cha TBC SONGEA chini ya Mtangazaji mahiri wa Kipindi cha Ulimwengu wa Vijana Komredi Shekhan wa Mzaina.
Mkuu wa shule hiyo Mzee Simon Maguru alizisikia pia taarifa za ushindi wa mwanafunzi wake huyo kupitia kituo hicho cha redio, pamoja na awali kuyabeza mashindano hayo kwa kuyaona ya kihuni, Mzee huyo wa makamo alionekana kupendezwa na taarifa hizo za ushindi wa mwanafunzi wake huku akiahidi kuungana na walimu wengine wa shule hiyo pamoja na wanafunzi wake kwenda kumpokea Vivian kwa maandamano makubwa.
Bendi ya shule ilipewa taarifa ya tukio hilo kubwa na tayari wanabendi walikwishajiandaa chini ya kiongozi wao wa bendi Jaston Mbawala ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha tano akichukua mchepuo wa HKL yaani (Historia, Kiswahili na Lugha)
Baada ya mipango yote kukamilika msafara kutoka katika sekondari ya Maposeni kuelekea katika Ukumbi wa Posta ambako kulifanyika mashindano hayo ulianza huku kila mtu akionekana kuwa na furaha isiyomithilika.
Wakati hayo yakifanyika shuleni Maposeni, upande wa pili wa shilingi Mzee Kanisius Matata, Baba mzazi wa Vivian Matata Mfanyabiashara maarufu wa kahawa wilayani Mbinga,anapata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama Mratibu wa mashindano hayo huku akimsifu na kumpa taarifa hiyo ya binti yake kuwa mshindi mpya wa mashindano hayo ya ulimbwende.
Jibu la Mzee huyo wa makamo linamtisha Mratibu huyo wa mashindano na kujikuta akishindwa kuendelea na mazungumzo, simu yake inaanguka chini na kujizima. Mmoja wa waandaaji wa mashindano hayo anaamua kuiokota simu hiyo na kuiwasha, baada tu ya kuiwasha unaingia ujumbe mfupi wa simu, anausoma ujumbe huo na kuonekana kuingiwa na mashaka, anaikabidhi simu hiyo kwa wenzake na kuwaonyesha ujumbe huo ambao unamtisha kila mmoja wao.
Amani inatoweka ndani ya mioyo yao kila mmoja anajikuta akibaki na mashaka, si ujumbe wa kawaida ni ujumbe wa kutisha unaoonesha wazi kuwa mtumaji amedhamiria kufanya kitu anachomaanisha.
******
Mzee Kanisius Matata
Alikuwa ni Mzee wa makamo aliyekuwa maarufu sana katika mji wa Mbinga, umaarufu wake ulitokana na utajiri mkubwa aliokuwa nao, utajiri uliotokana na zao la Kahawa ambapo alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa zao hilo akishirikiana na makampuni mbalimbali makubwa ya ndani na nje ya Mbinga.
Alishirikiana vema na mke wake Bi Siwema Matata aliyekuwa na elimu ya chuo kikuu. Shahada ya uchumi ya mwanamama huyo aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka mingi iliyopita ilikuwa msaada tosha katika kufanikisha malengo na mipango yote ya kuendesha biashara hiyo.
Walifanikiwa kupata mtoto mmoja tu katika maisha yao, hii ni baada ya Mama huyo kusumbuliwa na kansa ya mlango wa kizazi mara tu baada ya kumzaa mtoto huyo ambaye ni Vivian. Baada ya kupona Madaktari walimshauri kufunga kizazi na kutokuwa na uwezo wa kushika mimba tena.
Akiwa na umri wa miaka miwili mtoto wao huyo alionekana kuwa gumzo katika mitaa ya Uzunguni mtaa ambao Mzee Matata na mke wake walikuwa wakiishi katikati ya Mji wa Mbinga, kila mgeni aliyewahi kuwatembelea ilikuwa ni lazima awasifie wazazi hao kwa kumzaa mtoto mrembo na wa kuvutia yaani Vivian.
Kadiri siku zilivyozidi kwenda sifa hizi ziliendeleea kumiminika na kwa kiasi fulani Mzee Matata alianza kuboreka na sifa hizo, kwake aliziona sifa hizo kama uchuro kwa mwanaye huyo wa pekee, umri wa miaka miwili aliokuwa nao mtoto wao huyo haukustahili kuzungumziwa kila mara tena na watu wa rika lote, si wakubwa si Vijana.
“Zee Matata hii toto yako zuri sana aisee, itabidi iolewe na mwanangu Zuresh”
“Unasemaje wewe Mhindi koko?”
“Wewe tukana tu mimi ila mi sitaacha kukueleza wewe kweli yote, toto yako zuri sana bhana tangu nije Bongo sijawahi ona toto iliyoumbwa ikaumbika kama hii toto yako, toto ina shavu dodo, toto rembo sana hii, taleta posa mimi ili iolewe na mwanangu Zuresh, utataka mali ngapi?”
Mfanyabiashara maarufu wa kihindi mjini Mbinga alijikuta akishindwa kuuvumilia urembo wa mtoto huyo mdogo, mtoto wa pekee wa Mzee Matata. Maneno yaliyotoka kinywani mwa Mhindi huyo yalimkinaisha Mzee Matata ambaye hakuwa mtu wa utani, kwake maneno hayo hakuyatofautisha na matusi.
Alikuwa tayari afanyiwe utani yeye mwenyewe lakini si mtoto wake mpendwa aliyempenda kuliko kawaida, alishindwa kujizuia na kujikuta akimshushia kipigo mhindi huyo ambaye alikwenda kwake kwa ajili ya kuongea biashara ya kahawa lakini baada ya kumuona mtoto huyo alisahau kilichompeleka.
Ulikuwa ni ugomvi mkubwa kwani Mhindi huyo hakuwa tayari kukubali kupigwa kwani hakuona kosa alilokuwa amelitenda, kuweka oda ya posa kwa Mzee Matata kwake lilikuwa ni jambo la kawaida lakini kwa Mzee Matata yalikuwa ni matusi makubwa.
Mhindi wa watu alijaribu kutengeana ngumi na Mzee Matata, Mzee ambaye katika vita ya Kagera ya mwaka 1977 alikuwa akilitumikia Jeshi la Tanzania lililomfurumusha Rais wa Uganda kipindi hicho Hayati Iddi Amin ‘Dadaa’ katika kipindi hicho Mzee huyo alikuwa na cheo cha Sajenti, kitendo cha kutaka kujibu mashambulizi kiliongeza kasi ya mvua ya kipigo kutoka kwa Mzee Matata.
Ngumi ya taya pamoja na teke la kiunoni vilitosha kabisa kumfanya mhindi huyo aweze kusalimu amri mapema na kumuomba msamaha Baba mzazi wa mtoto mdogo Vivian. Ugomvi huo ulimshangaza sana Mama yake na Vivian lakini kwa upande fulani alikuwa upande wa mume wake kwani kipigo hicho kingekuwa funzo kwa wengine kuacha kumzungumzia mtoto wao mpendwa.
“Zee Matata sawa tu, umepiga mimi bila kosa yoyote, onevu sana wewe! Mimi naondoka ila yote namwachia Mungu”
Ndivyo ilivyokuwa! Siku ya pili mazungumzo kuhusu kipigo alichokipata Mhindi huyo yalisikika katika kila pembe ya Mji wa Mbinga huku baadhi ya watu waliokuwa na mazoea sawa na Mhindi huyo wakikata shauri la kutokumzungumzia mtoto huyo tena kwani kipigo hicho kilikuwa somo tosha kwao.
******
Walimlea mtoto wao kwa mahaba makubwa huku wakiahidi kumjengea msingi imara wa maisha yake ya baadaye, walimsisitiza sana kusoma kwa bidii ili mwisho wa siku aweze kuja kuishi maisha bora na yenye amani. Kwa bahati nzuri maendeleo yake shuleni yalitia fora kwani bidii yake katika taaluma sambamba na nidhamu aliyokuwa akiionesha tangu akiwa Chekechea vilimfanya aongoze katika kila mtihani aliokuwa ameufanya.
Alianza darasa la kwanza akiwa na umri wa miaka mitano na kumaliza kidato cha nne katika shule ya wasichana ya Mtakatifu Francis iliyopo jijini Mbeya ambapo matokeo yalipotangazwa alipata A katika kila somo na kupata daraja la kwanza na pointi 7. Baada ya matokeo hayo wazazi wake walitaka wampeleke jijini Dar es Salaam ili akasome katika shule maarufu ya Loyola kwa masomo ya kidato cha tano na sita.
Lakini tofauti na walivyotegemea, Vivian aliyapinga maamuzi hayo huku akiwaomba wazazi wake kusubiri mpaka serikali itakapompangia shule ya kwenda, lengo lake lilikuwa kusoma shule ya serikali ili kuweza kuyafahamu mazingira yote ya shule za binafsi na zile za serikali, aliwaeleza wazi kuwa alikuwa tayari kupambana na changamoto zote atakazokutana nazo na kuwataka wazazi wake kutokuwa na wasiwasi wa aina yoyote.
Hoja aliyoitoa mtoto wao huyo ilipingwa vikali na Mzee Matata, lakini baada ya jitihada zake za kumshawishi kushindikana ilibidi akubaliane na hali na kuamua kumkubalia mtoto wake huyo kwa shingo upande.
Vivian alifurahi sana, kwani aliamini kuwa huo ungekuwa wakati wake wa kuifahamu vizuri dunia tofauti na awali kwani alilelewa katika mazingira ya kufungiwa fungiwa sana tangu akiwa nyumbani mpaka shuleni kutokana na aina ya shule alizokuwa amepitia kuwa za geti kali sana.
Mwezi mmoja baadaye serikali ikatangaza majina ya wanafunzi waliofahuru na shule walizotakiwa kwenda kusoma masomo ya kidato cha tano na sita.
Vivian Matata alipangiwa katika shule ya sekondari ya Maposeni shule ambayo ilikuwa na michepuo ya masomo ya sanaa masomo ambayo msichana huyo alionekana kuyapenda kuliko kawaida, hii ilitokana na ndoto zake za kuja kusomea Uandishi wa Habari miaka ya mbele.
Pamoja na jitihada za wazazi wake kumtaka aende akasome masomo ya Sayansi, mtoto wao huyo aliwaeleza wazi kuwa hakuwa tayari kwani ndoto zake zilikuwa kuja kuwa mwandishi maarufu wa Habari nchini Tanzania huku akimtaja mwanamama Hanna Mahyige wa TBC kama role model wake yaani mtu anayetaka kufanana naye, kwa kutaka kuwa Mwandishi tayari ilimlazimu kusoma masomo ya Sanaa.
Wazazi wake hawakuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na maamuzi yake hayo ambapo baadaye alijiunga rasmi katika shule ya sekondari ya Maposeni, shule ya mchanganyiko iliyokuwa maarufu kwa kufaulisha katika masomo ya sanaa katika michepuo ya HKL, HGK na HGL, yeye Vivian alipangiwa mchepuo wa HKL yaani Historia, Kiswahili na Lugha.
Ujio wake sekondarini hapo ulikuwa gumzo katika kila mwanajamii wa shuleni hapo, si walimu wala wanafunzi kila mtu alionekana kuchizika vilivyo na uzuri wa Vivian, hali hii hata yeye mwenyewe ilimshangaza.
Siku zikazidi kusonga kwa kasi, hatimaye akaanza kuizoea hali hiyo taratibu, suala la kutongozwa na wanaume wa kila rika alikwisha lizoea na kila alipotamkiwa maneno ya ushawishi wa kimapenzi Vivian aliyakumbuka maneno ya wazazi wake hasa Mama yake mzazi aliyemweleza wazi kuwa Wanaume ni watu wabaya sana na wana maneno matamu ambayo ni rahisi sana kwa msichana kuhadaika na kujikuta akishindwa kutimiza ndoto zake.
Kila alipoyakumbuka maneno hayo wala hakuweza kumsikiliza mwanaume yeyote, aliwapenda sana wazazi wake na wala hakuwa tayari kuja kuwaumiza kwa kujiingiza katika mambo ambayo hata Baba yake mzazi alikwishamtahadharisha mapema. Ukali wa maneno ya Baba yake huyo ulimfanya aogope zaidi kujiingiza katika mchezo huo mbaya wa mapenzi.
Bidii yake katika taaluma ilizidi ile ya siku za nyuma kwani aliendelea kuwa kinara katika kila mtihani alioufanya shuleni hapo, mwaka ukakatika akaanza masomo mapya ya kidato cha sita huku wanafunzi wapya wa kidato cha tano wakiripoti tayari kuanza muhula mpya wa masomo.
Ubora wake katika masomo ulimfanya achaguliwe kuwa kiranja mkuu wa taaluma shuleni hapo huku akionekana kuwa na upeo wa hali ya juu katika uongozi.
“Msela wangu umekiona kile kifaa?”
“Kifaa gani tena mwana?”
“Acha uzuzu wewe, ina maana tangu uripoti hapa Skonga hujawahi kukutana na kile kifaa cha form six kinachosoma mchepuo wa HKL?”
“Unamzungumzia yule academic?”
“Yap yap, huyo huyo kumbe tupo pamoja, unamuonaje yule binti aisee?”
“Yule demu level nyingine wewe, mziki wake sidhani kama kuna anayeweza kuucheza hapa skuli”
“Mmmmh! Asikwambie mtu aisee yule demu bakora aisee, katika maisha yangu sijawahi kukutana na mwanamke aliyeumbwa akaumbika kama Vivian, kweli Mungu anajua kuumba jamani”
Jaston Mbawala na rafiki yake kipenzi Enock Longinus wanafunzi wapya wa kidato cha tano walijikuta wakiwa katika dayalojia ya aina yake, dayalojia iliyohusisha urembo wa Vivian Matata mwanafunzi aliyetingisha kwa urembo siyo tu shuleni hapo bali katika mji mzima wa Peramiho.
Wakati vijana hao wakizungumza, pasipo kutegemea mmoja wao anaitwa na msichana waliyekuwa wanamzungumzia, si kijana mwingine bali ni Jaston Mbawala .
Jaston haamini kama ni yeye ndiye anayeitwa, anaitika kwa sauti ya mashaka na kumuendea msichana huyo kwa mwendo wa kinyonge, anakutana naye uso kwa uso huku nyama za midomo ya juu na ya chini zikimtetemeka…………….
Je, msichana Vivian Matata anataka kuzungumza nini na kijana huyo? Na kwanini Kijana huyo anaonekana kuwa na hofu kubwa? Vipi kuhusu waratibu wa Miss Peramiho, waliambiwa na kutumiwa meseji gani na Mzee Matata?
Tukutane tena Ijumaa ijayo panapo majaaliwa!
Maoni/Ushauri nitumie kwenye namba hiyo hapo juu.
NINAWATAKIA WIKIENDI NJEMA WAPENDWA.
NINAWATAKIA WIKIENDI NJEMA WAPENDWA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni